Loading...

Timu ya Samatta Genk Yachapwa Goli 2 kwa 1, Samatta Acheza Dakika 45 Tuu


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amecheza kwa dakika 45 tu, timu yake KRC Genk ikifungwa mabao 2-1 na KV Oostende katika mchezo wa Ligi ya mchujo Ubelgiji kufuzu michuano ya Ulaya usiku wa Jumamosi Uwanja wa Schiervelde mjini Roeselare.

Samatta alitolewa baada ya kipindi cha kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Mgiriki Nikolaos Karelis, wakati huo Genk inaongoza 1-0 kwa bao la Mbelgiji Thomas Buffel aliyefunga dakika ya 25.

Lakini akiwa benchi, Samatta aliishuhudia Genk ikifungwa mabao mawili kipindi cha pili la kwanza na Mzimbabwe Knowledge Musona dakika ya 71 na la pili na Jordan Lukaku dakika ya 90 na ushei.

Samatta leo amecheza mechi ya 14 tangu ajiunge na Genk akitoka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na TP Mazembe pamoja na kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika.

Katike mechi hizo, ambazo saba tu ndiyo ameanza, mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam, amefunga mabao nne, moja katika kila mechi Genk ikishindia 2-1 ugenini dhidi ya wenyeji SV Zulte-Waregem, 4-0 na 4-1 dhidi ya KV Oostende na 3-2 dhidi ya Club Brugge mchezo wa kwanza.

Majipu Mapya Tume ya Uchaguzi naTanesco Yaibuliwa Bungeni


Ripoti ya mwaka ya Mamlaka ya Udhibiti wa Umma (PPRA) imewasilishwa bungeni mjini Dodoma ikibainisha majipu katika utoaji wa zabuni katika baadhi ya mashirika na taasisi za umma ikiwamo Tume ya Uchaguzi na Tanesco.

Ripoti hiyo ya tathimini kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 iliyotiwa saini na mwenyekiti wa bodi, Balozi Dk Martin Lumbanga iliwasilishwa juzi na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashantu Kijaji, ikibainisha ukiukaji wa taratibu za zabuni, harufu ya rushwa na kupuuzwa kwa ushauri wa mamlaka hiyo.

Ununuzi wa BVR

Katika ripoti hiyo mamlaka hiyo inabainisha majipu kwa kutofuatwa kwa kanuni katika zabuni ya ununuzi wa vifaa vya kuandikisha wapiga kura (BVR).

Imeelezwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilipotangaza zabuni hiyo ya Dola 78.9 milioni (Sh 169.6 bilioni) kampuni ya SCI Tanzania Limited ilishinda zabuni hiyo lakini ikalalamikiwa.

Katika malalamiko yake, kampuni ya Safran Morpho ambayo pia iliomba zabuni hiyo, ilikata rufaa ikisema haikuridhishwa na mchakato mzima ulivyoendeshwa na SCI Tanzania Limited kushinda.

Baada ya kushughulikia rufaa, Mamlaka ya Rufaa ya Manunuzi ya Umma (PPAA) ilibaini kuwa SCI Tanzania Ltd haikuwa na uzoefu uliotakiwa, fedha, ufundi wala uwezo wa kuzalisha na ikaiagiza NEC kuanza mchakato wa zabuni upya.

Badala ya kutekeleza uamuzi huo, NEC iliwakaribisha tena wazabuni wote ambao walishindana katika zabuni iliyofutwa na vifaa vya kampuni ya Lithotec Export vilionekana kufanya kazi vizuri.

Ripoti hiyo inasema NEC iliamua kutumia utaratibu wa chanzo kimoja (single source) na kusaini mkataba na kampuni hiyo ya Afrika Kusini ya kusambaza BVR 10,500 zenye thamani ya Dola za Marekani 89 milioni (Sh191.3 bilioni), ikiwa ni ongezeko la Sh21.7 bilioni za awali.

Mbali na hilo, baadhi ya maofisa wa NEC walishiriki katika timu ya uthamini kwenye bodi ya zabuni na vikao vya majadiliano, hali iliyosababisha mgongano wa maslahi.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhan alipoulizwa alisema sheria ya manunuzi ya umma inaruhusu kupatikana mzabuni kwa njia ya ‘single source’ na kwamba hawakuwa wamevunja sheria yoyote na BVR 8,000 zilinunuliwa na watu wakapiga kura.

“Ni kweli PPAA walipoona mapungufu walitwambia turudie mchakato upya na sheria inaruhusu mzabuni mmoja kulingana na mazingira, hatukuwa kinyume cha sheria,” alisema Kailima.

Majipu Rahco

Katika hatua nyingine, PPRA imebaini madudu katika zabuni ya kuboresha Reli ya Kati iliyofanywa na kampuni ya Rahco, ambayo haikuwa katika mpango wa manunuzi kwa mwaka 2014/2015.

Mamlaka hiyo inadai mkurugenzi mkuu wa Rahco alijitwalia madaraka yote ya kuwa mamlaka ya uidhinishaji wa bajeti na yale ya bodi ya zabuni na kuidhinisha matumizi ya fedha.

Meneja mkuu wa manunuzi wa Rahco, alitoa ushauri sahihi kwa mkurugenzi huyo mwendeshaji lakini ushauri wake haukuzingatiwa na matokeo yake alibanwa na mkurugenzi huyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bodi ya zabuni ya Rahco haikushirikishwa kabisa katika mchakato huo wa zabuni ambapo kampuni ya CRCC and Integreted Communication zilipewa zabuni.

Jukumu la kuita wazabuni na kuwapa zabuni hiyo lilifanywa na mkurugenzi mwendeshaji wa Rahco pekee bila kushirikisha bodi ya zabuni, taarifa hiyo inabainisha.

PPRA imeeleza katika taarifa hiyo kuwa hakuna ushahidi wowote wa nyaraka kuonyesha ni kwanini mkurugenzi huyo aliivunja bodi ya zabuni iliyokuwepo na kuteua nyingine kabla ya muda wake kwisha.

Mamlaka hiyo imependekeza mkurugenzi huyo, Benhadard Tito afike mbele ya Bodi ya wakurugenzi ya Rahco kujieleza ni kwanini alikiuka kwa makusudi sheria ya manunuzi ya umma.

Vilevile mamlaka hiyo inaagiza bodi ya wakurugenzi kumchukulia hatua mkurugenzi huyo huku ikipendekeza suala hilo lipelekwe Takukuru ili kuchunguza uwepo wa mazingira ya rushwa.

Mamlaka hiyo ilipendekeza Rahco ijulishwe kuwa zabuni kati yake na makampuni hayo ni batili na ianzishe mchakato upya na pia kulipeleka suala hilo kwa mkurugenzi wa upelelezi (DCI) kwa uchunguzi zaidi.

Hata hivyo, Tito na mwanasheria wa Rahco, Emmanuel Massawe na mwakilishi wa kampuni ya RothChild Proprietary Ltd ya Afrika Kusini, Kanji Mwinyijuma wameshtakiwa kwa makosa tofauti na hilo la PPRA.

Tito ameshtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka na kula njama na kuisababishia Serikali hasara ya Dola 527,540 za Marekani.

NHIF na kampuni ya China

PPRA inabainisha kuwa zabuni ya Sh8.1 bilioni ilitolewa kinyume cha taratibu na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kampuni ya China Wuyi Co. Ltd.

PPRA inasema NHIF kupitia barua yake ya Agosti 28,2014, iliitaka mamlaka hiyo kufanya uchunguzi katika mchakato wa zabuni hiyo ikishuku kuwapo kwa mchezo mchafu.

Baada ya uchunguzi, PPRA ilibaini kuwa timu ya wathamini ya NHIF ilikosea kwa kupendekeza kampuni hiyo ipewe zabuni kwa sababu ilikuwa imefungiwa na Benki ya Dunia kufanya shughuli za manunuzi kuanzia mwaka 2009 hadi 2017.

Kutokana na makosa hayo, PPRA imemtaka ofisa aliyehusika kusaini zabuni hiyo kujieleza kwanini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kukiuka sheria kwa kuipa zabuni kampuni iliyozuliwa kushiriki manunuzi ya umma.

Pia mamlaka hiyo imependekeza kuchukuliwa kwa hatua kwa timu ya uthamini kwa kushindwa kubaini mapungufu hayo na hatua kama hizo pia zichukuliwe kwa bodi ya zabuni ya NHIF.

Tanesco na zabuni ya mafuta

Mbali na suala hilo, mamlaka hiyo pia imemtaka mwenyekiti wa bodi ya zabuni ya Tanesco kujieleza kwanini asichukuliwe hatua kwa kuiingiza kampuni ya Camel Oil (T) Ltd katika zabuni wakati iliondolewa kwa kukosa sifa.

Kampuni hiyo pamoja na Oryx Oil Company Limited ziliingizwa katika zabuni ya ununuzi wa mafuta mazito (HFO) kwa ajili ya mashine za kuzalisha umeme za kampuni ya IPTL.

Ripoti hiyo inafafanua kwamba shehena ya kwanza ya lita milioni 9 zenye thamani ya Sh12.4 bilioni zilinunuliwa kutoka kampuni ya BP na shehena ya pili ya lita milioni 16 yenye thamani ya Sh21.2 bilioni ikanunuliwa kutoka Puma.

Hata hivyo, PPRA imebaini mapungufu ikiwamo kutokuwapo kwa barua ya ushindi wa zabuni iliyotumwa kwa BP na pia hapa kuwa na hati ya makabidhiano (delivery note) kama ushahidi.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa kampuni ya BP ililipwa kwa kuegemea mzigo uliopakiwa wa lita 8,979,000 lakini shehena iliyoshushwa katika mitambo ya IPTL ilikuwa lita 9,970,106, ikiwa ni lita 991,106 zaidi.

Mamlaka hiyo ilibaini kuwa kutokana na zabuni hiyo, BP ililipwa Sh12.4 bilioni kwa hati ya malipo namba 58 VC 1100081 ambayo ilionyesha malipo hayo yalizidishwa kwa Sh42.4 milioni

Jaji Mkuu: Sheria Ya Makosa ya Mtandaoni Haina Lengo la Kuwakandamiza Watanzania


JAJI MKUU wa Tanzania, Mohammed Chande Othman amesema sheria ya mitandao ilipitishwa kwa lengo jema la kulinda watumiaji, wanajamii na usalama wa Taifa la Tanzania.

 

Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Mei 14, 2016) wakati akijibu baadhi ya maswali kutoka kwa Watanzania waishio Uingereza kwenye mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini London, Uingereza.

 

Alisema watu watatu kati ya wanne nchini Tanzania wakiwemo watoto, wanamiliki simu za mkononi ambayo ni sawa na watu milioni 35 kati ya milioni 45.

 

Alisema sheria hiyo ilitungwa kwa misingi mitatu moja ikiwa ni kumpa mtumiaji uhuru wa kutoa maoni au taarifa, uhuru ambao alisema unalindwa kikatiba lakini akaonya kuwa kila uhuru unaotolewa pia una mipaka yake kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 30(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Alisema sheria hiyo pia inatoa uhuru wa mtu kuwa na faragha (privacy) na msingi wa tatu ni sheria hiyo kuzingatia matumizi ya mitandao ili kulinda usalama wa nchi.

 

“Sheria hii inakupa uhuru wa kutumia mtandao kumlinda mwanajamii wenzako. Hapa Uingereza nimeongea na mwendesha mashtaka mkuu ambaye aliniambia kuwa asilimia 60 ya makosa yanayofanyika chini ya sheria ya makosa ya kujamiiana (S3x.ual Offencea Act) yanatokana na mitandao,” alisema Jaji Mkuu wakati akijibu swali kuhusu sheria ya makosa ya mitandao.

 

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga alisema kuitishwa kwa mkutano wa kupambana na rushwa nchini Uingereza ni mojawapo ya jitihada za Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuanzisha vuguvugu la uanaharakati wa mapambano dhidi ya rushwa.

 

“Kukosekana kwa utawala bora, changamoto za ugaidi, biashara za dawa za kulevya, biashara ya kusafirisha binadamu na uwepo wa rushwa na ufisadi ni baadhi ya mambo yaliyofanya dunia ibadilike. Haya mambo zamani yalikuwa hayana mahali pa kuzungumzwa, kwa hiyo vikao kama hivi vitasaidia kukabili tatizo hili,” alisema.

 

“Rushwa ni kama pweza mwenye vichwa vingi na mikia mingi. Waziri Mkuu David Cameron ameamua kuanzisha movement hii ili kutafuta njia za kukabili janga hili kubwa,” alisema.

 

"Sote tunatambua kuwa mataifa mengi yangependa kuwemo katika hii movement lakini ni faraja kuona kwamba Tanzania imo miongoni mwa waanzilishi na hii ni kwa sababu ya uongozi na ujasiri wa Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye kwa kweli ni game changer  (akimaanisha kuwa amebadili mwelekeo wa Taifa hili) kwani ana utashi wa kisiasa na ana ujasiri wa kukemea maovu,” alisema huku akishagiliwa

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Valentino Mlowola alisema vita ya rushwa nchini Tanzania ni endelevu na inafanyika kuitikia wito alioutoa Rais Magufuli wakati akizindua Bunge la Tanzania Novemba 20, 2015.

 

Alisema wanatumia mbinu mbalimbali kupambana na rushwa lakini kubwa wanayoenda nayo hivi sasa ni kutoa elimu kwa watoto na vijana ili kuwabadilisha tabia na utamaduni uliojikita kwenye jamii.


IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU

JUMAPILI, MEI 15, 2016.

Nilikuwa Silipwi Kitu Top Band Kwa TID - Ommy Dimpoz Afunguka


Msanii Ommy Dimpoz amesema wakati anaanza muziki alipokuwa Top Band, alipitia magumu ambayo ndiyo yamemjenga.

Ommy Dimpoz ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Radio, na kusema kuwa hajayajutia magumu hayo, kwani alikuwa anajifunza.

“Mwanzo wakati naanza nipo Top Band nilikuwa siko vizuri financially (kifedha), nilikuwa sina hela, nilikuwa naenda kwenye shoo kwenye bendi, ilikuwa some times (wakati mwingine) tunapata, unajua nilikuwa najifunza kama unaenda gereji, unaweza ukaitengeneza gari yote mwenye fundi anakuelekeza alafu hela yote anachukua, lakini kama unaelewa hapa nipo najifunza utaona kawaida utasema hapa nipo najifunza”, alisema Ommy Dimpoz.

Ommy Dimpoz kwa sasa anamiliki lebo yake na kampuni yake ya Poz kwa Poz (PKP), na ameanza kwa kusaidia kuibua wasanii wachanga akiwemo Nedy Music, kitu ambacho alinukuliwa akisema kilikuwa ndoto yake ya siku nyingi

Waroho wa fedha kupewa mkono wa kwaheri Simba


Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, ametamka wazi kuwa wachezaji wote wanaoweka fedha mbele na wasiokuwa na mapenzi na timu hiyo hawatakuwa nao msimu ujao kwakuwa ndiyo wamechangia timu hiyo kukosa ubingwa wa msimu huu.

Hans Poppe ameyasema hayo baada ya hivi karibuni baadhi ya wachezaji wa Simba kugoma kwenda Songea kucheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Majimaji wakishinikiza kulipwa mishahara yao.
Wachezaji waliogoma ni wale wa kigeni ambao ni Hamisi Kiiza, Juuko Murshid, Emery Nimubona, Justice Majabvi, Vincent Angban, Brian Majwega na Paul Kiongera, lakini baadaye Majabvi na Angban waliungana na timu japo Angban akucheza kabisa huku Majabvi yeye akiingia kipindi cha pili.

Hans Poppe amesema: “Hatutaendelea kuwa na wachezaji wasiokuwa na mapenzi na timu, haiwezekani mshahara uchelewe kidogo halafu unagoma, mbona hata serikalini mishahara inachelewa na watu wanafanya kazi kama kawaida huku wakifuatilia haki yao kwa utaratibu lakini kwa wachezaji wa Simba imekuwa tofauti wamekuwa wakicheza ilimradi nakupelekea matokeo mabovu kwa timu hiyo na sasa imepoteza tena nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa kwa msimu wa nne.

Poppe ambaye kwa sasa ndiyo kama mhimili wa timu hiyo amesema “Hii haipo Simba tu, wanapaswa kutambua kwamba wapo kwa ajili ya kuipigania timu na masuala hayo yakitokea si sisi bali mazingira ndiyo husababisha, bora tubaki na wachezaji wenye mapenzi na timu kuliko wa aina hii awana uchungu na timu.”

"Hebu angalia sasa wamelipwa na walicheza kinazi na timu imepoteza nafasi ya ubingwa na uwakilishi wa michuano ya Kimataifa sasa hiyo mishahara wameifanyika kazi gani wakati wameharibu," alihoji Hans Poppe.

Kauli hiyo ya Hans Poppe inamaanisha kuwa, Kiiza na Juuko wana nafasi ndogo ya kubaki Simba kwani huwa hawataki kucheleweshewa mishahara yao.

Kiiza amekuwa akilaumiwa kwamba amekuwa chanzo cha migogoro ya chini chini ndani ya klabu hiyo hali inayosababisha mfarakano kati ya wachezaji na viongozi na kupelekea timu hiyo ambayo ilikuwa katika mbio za ubingwa kupoteza mwelekeo dakika za mwisho na kutoa mwanya wa mahasimu wao Yanga kuendelea kutamba.

Hivi karibuni, Kiiza aliwahi kufukuzwa kambini kutokana na utovu wa nidhamu na uamuzi huo ulichukuliwa na meneja wa Simba.

Simba sasa baada yakupoteza mwelekeo kutokana na kukosa mshikamano baina ya wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na wanachama wamekuwa katika malumbano ya chini chini baina yao huku mashabiki na wanachama wakipiga kelele na kupaza sauti zao kuutaka uongozi wao ujiuzuru ama uitishe mkutano mkuu wa dharula kujadili mustakabali wa timu hiyo.

Mashine "iliyotumbuliwa" na JPM Uwanja wa Ndege Imepona na Inafanya kazi Kwa Ufasaha


Hatimaye mashine iliyotembelewa na Rais JPM jana na kukutwa ikiwa mbovu au haifanyi kazi kwa ufanisi sasa inapiga mzigo kama kawaida na ikiwa chini ya uangalizi wa Maafisa Usalama wa Mamalaka ya Viwanja vya Ndege,Polisi na Afisa wa TRA.

Mashine hiyo aina ya Rapscan inayotumika kukaguwa mizigo ya abiria wanaoingia Dsm kutoka Znz,na mikoa mingine ya Tanzania,mapori ya Utalii kama Selous,Mikumi,Sadani na Ruaha pamoja na wasafiri wa nje ya nchi.Ikumbukwe kuwa palikuwa na "uzembe" wa abiria wanaoingia nchini kupitia eneo la TB One,uwanja wa Terminal One una "Status" ya "General Aviation" kwa maana huruhusu kutua ndege za abiria,mizigo na kukodishwa,ambazo zinaweza kuwa za kutoka ndani ya nchi au nje ya nchi

Kwa maana hiyo,Arrival ya Terminal One ni tofauti na ile ya Terminal Two,sababu ya Teeminal Two imegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni "Domestic Arrival" na "International Arrival",hivyo ndege nyingi za domestic katika Terminal Two mizigo ya abiria haina haja kukaguliwa sababu watu wanatoka mkoa mmoja ndani ya nchi kwenda mkoa mwingine,na wale wanaotoka nje ya nchi hawachanganyikani na wa ndani ya nchi

Uwanja wa Terminal One "Arrival" hiyo hiyo moja hutumika na abiria wa kutoka Zanzibar,Mikoani,Mbuga za Wanyama(Porini) na nje ya nchi.Hivyo kuwa na Mashine mbovu eneo la Arrival ambayo inahudumia watu wanaopita toka Zanzibar(Wakiwa na mizigo ya kibiashara kwa nia ya kukwepa ushuru) na nje ya nchi ni "kosa" kiutendaji.Wapo watu kama Pasco wa JF wanaodhani JPM kakurupuka,wasijuwe kuwa "status" ya Terminal One Arrival sio kama ile ya "Domestic Terminal Two"

Vijana wa JPM,hatumpi vitu vya kukurupuka,anapewa data zilizoshiba,ndio maana akifika anaenda moja kwa moja.Jana baada ya kuongea tu kufika saa kumi mashine zikawa zimetengenezwa na mizigo inakaguliwa kwa ufanisi mkubwa.Simu nyingi zilizokuwa zinapitishwa kinyemela toka Dubai via Zanzibar kuja Dsm zimeanza kunaswa,mali pori zisizo na vibari zinaonekana na hivyo kuwa na uhakika wa kutambua nini na nini kinaingia nchini.

Kwa taarifa tu ni kuwa Wamiliki wengi wa ndege Terminal One ni wafanyabiashara wa uwindaji na utalii,matengenezo ya ndege zao hufanyika nje ya nchi,hivyo hufanya udanganyifu wa kwenda porini na kubeba mali pori,kurudi Dsm bila kuushusha mzigo,na baadae kusafiri kwenda nje ya nchi na mzigo "kimyakimya",na wakati ndege zikirudi toka nje huja na bidhaa ambazo ni "dutable",na baadae kuingia nchini bila kutozwa kodi

Ujanja mwingine uliokuwa unatumika na wafanyabiashara wengi ni kushusha mzigo Zanzibar na baadae kuuleta Dsm na ndege za Charter na hivyo kukwepa kosi,Ndege ya Qatar na Oman Air hutua Zanzibar,hivyo wafanyabiashara wengi huja na bidhaa na kuzishusha Znz na baadae wanakuja kama abiria kupitia Terminal One na hivyo kuingiza nchini bidhaa nyingi bila kulipa kodi,kwa mashine ile kutokutumika vizuri basi Taifa limepoteza mapato mengi kwa muda mrefu

JPM kwenda pale jana hajakurupuka,ni matokeo ya jitihada za kumuonyesha sehemu ambapo kuna mianya ya ukwepaji kodi.., Twende JPM ipo siku watakuelewa,hasa utakapoanza kuiachia hela unayoikusanya sasa,wacha tule ugali dagaa kwa muda..Msosi wa uhakika mezani unakuja

By Barafu

Haya Mambo Yafuatayo Huwafanya Wanawake Wengi Kushindwa Kuingia Katika Ndoa (Kuolewa)


Pamoja na kuwa kuna wanawake husita kuolewa, lakini jambo hili si kubwa sana kwa wanawake kama ilivyo kwa wanaume. Kwa kiasi kikubwa katika suala la kutaka kuingia ndani ya ndoa, wanawake ni wengi ambao hutaka kufunga ndoa kuliko ilivyo kwa wanaume. Hilo tunaliona wazi tokana na shamra shamra awazo nazo mwanamke wakati wa maandalizi ya shughuli za Ndoa na Harusi.

Hata hivyo, kwa wale wanawake wachache ambao husuasua kuolewa hizi ni baadhi ya sababu zinazopelekea kusuasua huko. (Izingatiwe hii ni kwa wanawake ambao hawajawahi kuolewa kabisa)

Vigezo vilivyopitiliza viwango (hasa kwa muonekano)
Wanawake wengi hasa wa umri mdogo (lakini unatosha kuolewa) hutumia muda mwingi katika kuchagua aina ya mwanaume ambaye angependa awe mume wake. Wanawake hawa hujiamini zaidi na kusimamia sifa zile ambazo huamini ni muhimu mwanaume wa kumuoa awe nazo.  Vigezo hivyo huwa hata kwa misingi ya muonekano wa mwanaume huyo – kuna wale ambao hutaka mwanaume huyo wa kumuoa awe na sifa kama vile, mrefu, aliyejazia kifua, mtanashati, sauti nzuri n.k. Inaweza kuwa kama mzaha na ikaonekana ni kipengele kidogo sana lakini bado kuna wale ambao anaweza kuwa tayari kuolewa ila hataki sababu tu huyo mwanaume hafananii vile ambavyo yeye anataka mumewe awe.

Kutaka mwanaume tajiri
Kuna wanawake ambao tayari wameshajiwekea akilini kuwa hatakubali kuolewa na mwanaume yeyote yule ambaye hana pesa nyingi. Yupo tayari kuolewa ila si kwa mwanaume mwenye uwezo wa kawaida – hata ikitokea mwanaume ana uwezo kidogo wa kuweza kujitosheleza, yeye bado huona huyo mwanaume hamfai hadi pale tu atakapo pata yule ambaye anahisi ataishi maisha ya kifahari. Hivyo hukazana kusubiri na kujitahidi kuwinda aina ya mwanaume ambaye atakuwa na uwezo mkubwa, bila kujalisha kama huyo mwanaume kampita sana umri.

Kutompata Mwanaume Ampendae
Hili ni kama tu vile ilivyo kwa wanaume ambao huamini ndoa haiwezekani na haifai bali tu hadi pale umpatapo yule ambaye unampenda na unaamini anakupenda pia.  Wengi katika kundi hili huamini kuwa mafanikio ya ndoa kigezo kikubwa ni kupendana tu na mengine hufuata kwenye sababu ya upendo. Kuna wanawake vigezo vya mwanamme awe vipi havina umuhimu kabisa katika kutaka kuamua kuolewa. Yeye kikubwa anataka ampate mume ambaye atampenda kwa dhati na huku akiwa na matumaini kuwa huyo mume atampenda na yeye pia kwa dhati.  Huyu mwanamke anaamini msingi bora wa ndoa ni mapenzi ya dhati kati ya yeye na mmewe basi! Hana haraka hadi pale atakapompata mwanaume akampenda ndipo atakapokuwa tayari kuolewa. 

Kuchagua mno Wanaume wa Kumuoa
Kuna wale wachache ambao akili hubadilika kama kinyonga; wasioridhika wala kujitambua ni nini wanataka ama mwanaume wa aina ipi wanataka. Akija wa mwenye uwezo atasema nataka wa kuchuma nae, akija asiye na uwezo atatoa sababu tu hata kama kumlaumu kuwa inaonyesha hajitumi kutafuta maendeleo. Akija wa kabila hii, atasema hapana hao wana tabia hii mimi siitaki! Yaani kwa ufupi ni mtu asiyeisha kutoa kasoro za wale ambao wanajitokeza kutaka kumuoa. Hatimaye inaweza tokea muda wa kuolewa ukapita na akaishia kupunguza uchunguzaji lakini ikiwa hata wanaume wa umri wa kufaa kumuoa kutokuwepo tena katika soko.

Kujiona ni mzuri sana
Kuna wanawake ambao ni kweli Mwenyezi Mungu kawajaalia uzuri hasa (uzuri wa muonekano), anakuwa ni mzuri kiasi kwamba wake kwa waume wote wanamkubali kwa uzuri huo na hata wote kumtamani. Hata hivyo hapo hapo kuna wale ambao huwa ni wazuri kawaida – ila kwa mtazamo wake hujiona ni mzuri mno hakuna mfano kama yeye; kitendo ambacho kwa wachache kwenye kundi hili hufanya kujiona yeye ni yeye na kuwa kwa yeyote kuwa na yeye huyo mtu anatakiwa atambue kuwa ana bahati sana. Kitendo hiki hukuza nyodo za hali ya juu ya mwanamke mwenye mtazamo huu, kiasi kwamba wanapojitokeza wanaume kutaka kuoa – anaweza onyesha tabia kama maringo, dharau na kiburi.

Kujiona ana Umri mdogo
Binti yeyote wa miaka 18 na kuendelea anaruhusiwa kuolewa endapo tu karidhia kuolewa. Wanawake wametofautiana mipangilio yao ya kimaisha, kuna wale akiwa katika umri wa kuolewa hutamani sana kuolewa na kuna wale ambao hupenda kuolewa wakiwa wakubwa zaidi. Katika kundi hili umri kuwa mdogo hutegemeana, kuna mwingine anakuwa na umri wa miaka 25 na bado akajiona mdogo na hali kuna mwingine anakuwa na miaka 20 na akajiona ni mkubwa na anafaa kuolewa. Hii pia ni kwa wanawake wale ambao huwa na malengo ya kutotaka kuharakisha katika ndoa. Anapokuwa na umri ambao anaweza kuolewa lakini yeye hayupo tayari kwa muda huo, huwa ni kikwazo kwake kuingia katika ndoa.

Maradhi hasa UKIMWI
Hili kama lilivyo kwa wanaume -  Pamoja na kuhamasishwa kwingi na wataalamu wa maradhi ya HIV/AIDS kuwa mtu hata ukiwa umeathirika unaweza kuwa na mahusiano na hata kuoa na kuwa na watoto; bado haisaidii sana kwa vijana wanaojitambua kuwa ni waathirika wakiwa bado ni wadogo, hawajaoa/olewa ama kuwahi kuwa na mtoto.  Wengi sana hukata tamaa na huona ni kheri kubaki walivyo kuliko kuingia katika ndoa, hasa tokana na imani kuwa wanawake wakizaa wakati ni waathirika; afya hudhoofika zaidi.

Kutaka maisha ya Tamthilia (Ndoa za kuishi kwa furaha milele)
Kutokana na kukua kwa idadi ya tamthilia nyingi ambazo huonyesha maisha ya kimagharibi zaidi; kumekuwa na dhana kwa baadhi ya wanawake kutaka hayo maisha ya tamthilia yawe na kwao pia. Hilo linafanya vigezo ambavyo mwanamke huyo anatumia kuchagua ama kukubali mwanaume kumuoa kutotimiza yale ambayo yeye binafsi anatarajia.  Wengi hushindwa kutambua kuwa hakuna maisha ya furaha milele, na hasa kuwa maisha ya maigizo yapaswa kuchanganya na zako kuweza kufanya maamuzi ya kipi kiigwe na kipi kiachwe kama kilivyo.

Kuona taasisi ya Ndoa kama Utumwa
Mtazamo huu kwa wanawake wenye msimamo huu, huchangiwa na baadhi kama haya:
- Usomi: Aina ya usomi ambao hupelekea kwa baadhi kuwa na tafsiri tofauti juu ya ndoa, haki, majukumu na mengine mengi.
- Kushuhudia ndoa mbovu: Hii inaweza kuwa ya wazazi/walezi wake wenyewe (pengine mama aliteswa sana), na hata ndugu wa karibu kama vile kushuhudia kila ndoa ya ndugu yake anayoijua mwanamke huishi kwa mateso, manyanyaso na maisha ya taabu na kuonewa.
- Kuwa na uwezo sana wa kujitosheleza ambao unaweza kumtimizia na kufanya lolote lile ambalo anataka katika maisha. Kwake kuwa na mwanaume kama mume kwake anaona kama ni utumwa.

Kutokuwa kabisa na mshipa wa hisia za kufanya mapenzi
Kuna wanawake wale wachache waliozaliwa hivyo. Hawana hisia yoyote ile ya kimwili ya kuweza kupata hisia za kuweza kujisikia ama kutamani kufanya mapenzi. Wengi wa aina hii ya wanawake huwa ni waoga sana wa kuwa karibu na mwanaume, na kwa wale ambao wamewahi hata jaribu baadhi huona kama kitendo cha ndoa ni kero, unyanyasaji na uchafu.  Hivyo wazo la kuwa akiolewa anatarajia kufanya kitendo cha ndoa mara kwa mara kinamvunja kabisa hamu ya kutaka kuolewa.
Older Posts
© Copyright bongonews | Designed By JAMIIYETUBONGO.COM
Back To Top